Nov 2, 2008

Taifa linaangamia taratibu chukua hatua




SALAAM Rais wangu Jakaya Mrisho Kikwete, nakusalimia ewe mtukuka mwenye nyingi rehema, mwenye upendo na nchi yako na watanzania wote hakika unaupendo mkubwa na nchi yako ndiyo maana huachi kufanya ziara kuizungukia nchi yakoTanzania kila sehemu ili kujua hari ya watu wako mlezi wa Tanzania na juzijuzi ulikuwa Mbeya, haya yote ni kutokana na kuipenda nchi yako.

Nchi yako Tanzania nayo Mungu ameijalia sana kwani rasilimali za kila aina vyote ameipatia, Tanzania tuna madini ya kila aina yakiwemo dhahabu, almasi, ulanga, Tanzanite n.k.

Vilevile ina maziwa na mito ya maji ya kila aina likiwemo ziwa vicktoria ambalo linazalisha samaki aina ya sangara kwa wingi ambao wakazi wa kanda ya ziwa wanapata Mapanki kwa ajili ya kutumia kama mboga kwani minofu yote huwa inachukuliwa na wawekezaji tuliowapa wachukue ili watupatie pesa za kigeni kwa maendeleo ya taifa letu.

Pamoja na hayo vilevile nchi yako Mheshimiwa Rais ina Milima mingi ukiwemo Mlima Kilimanjaro ambao ni Mlima mrefu kuzidi Milima yote Afrika, Mlima huu huwa unatuingizia pesa nyingi za kigeni yote haya ni kutokana na Mungu kuijalia nchi yako Tanzania.

Rais wangu Tanzania yako ina rasilimali nyingi sana ambazo na sisi watanzania tunazitumia ili kujiletea maendeleo pamoja na kwamba wawekezaji ndio wamechukua sehemu kubwa ya rasilimali zetu lakini yote haya ni kuhakikisha taifa linapiga hatua kimaendeleo.

Rais wangu Jakaya nakupa pole sana kwa Masaibu yaliyokukuta kwani tangia ukumbwe na kimbunga cha kuzomewa na kurushiwa mawe huko Mbeya sijakusalimia na kukupa pole baba mlenzi, mtetezi wa wanyonge.

Pole sana Mtukufu mlezi wa rasilimali za taifa kwa manufaa ya kizazi kijacho hakika wewe ni Mkombozi wa Tanzania ndio maana tulikupa kura kwa asilimia kubwa huku tukishangilia kuwa wewe ni chaguo la Mungu.

Yawezekana na Mungu alikujua kuwa wewe ndiye utakuja kuwatetea Watanzania kuondokana na dhuluma, unyonyaji, na kukomesha ufisadi ndani ya nchi yako mpaka kipindi cha miaka yako mitano itakapoisha ili kuingia tena uchaguzi mwingine wa hapo mwaka 2010 ambapo pia ungemalizia yaliyobakia.

Nakupa pole Rais wangu kutokana na matukio yanayoiandama serikali yako kwa sasa ni ya kusikitisha mno kwa sababu yanaashiria kuwa nchi yako Rais wangu ipo kwenye dimbi la hatari kuelekaea katika hari isiyo ya kawada kwani fikra za watu na hisia zao wameanza kuzionyesha hadharani sijui ni kwanini wanapata msukumu huu mpaka wa kuamua kukurushia mawe Rais wangu na kufanya Migomo ya kila aina?

Rais wangu yakupasa kufikiria kwa kina jambo hili la kurushiwa mawe wakati ukiwa katika ziara yako Mkoani Mbeya kwanini watu wa huko walidhubutu kukurushia mawe? Hapa kuna kitu ambacho unatakiwa kukitambua mapema ili kukipatia ufumbuzi kwa haraka zaidi kwani kitendo cha kukuzomea na kukurushia mawe ni nguvu ya fikra ya watu hao ya kufikria kuwa hujawatendea kitu fulani ambacho ulitakiwa kukitekeleza.

Sasa baada ya kuona kuwa haki yao hawapati japo kuwa ile haki wanaijua kuwa ni yao kihalali sasa ili kufikisha ujumbe wa hisia za fikra zao wakaamua kukuzomea na kurusha mawe ili ujue kuwa hujawapatia kile walichokuwa wanakitaka.

Nikiwa kule Mbeya kama kawaida yangu ya kuchukua habari ili nihabarishe umma wa Watanzania wenzagu wenye nia ya kujua matukio yanayotokea katika dunia hii nilibahatika kushuhudia kuzomewa kwa Rais Kikwete katika maeneo ya Mwanjelwa, katika maeneo hayo wananchi walipouona msafara wa wake walitanda barabarani kuuzuia msafara huo wa Rais wakimtaka azunguze nao.

Lakini alipojitokeza wananchi walianza kupiga kelele wakizungumzia ufisadi huku wakisema kwa nini Rais hashughulikii mafisadi mbalimbali wakiwemo wa EPA wakati aliapa kuwa atailinda na kuitetea katiba ya nchi? Na baadhi ya watu wakihoji kuhusiana ahadi alizotoa za kuwapatia ajira na maisha bora.

Na katika kijiji cha Kanga Wilayani Chunya tukio la kurushiwa mawe msafara wake ni jambo ambalo halisitahili na la kushangaza, lakini Rais wangu alichukulia kama jambo dogo na kumtaka Mkuu wa Mbeya John Mwakipesile ambaye alionekana kufadhisha sana na jambo hilo kwa kumwambia kuwa, asifadhaike sana kwani yeye Rais watu wa Mbeya wanampenda sana.

Rais jambo hili ni jambo zito kwani wananchi hawa kuamua kukurushia mawe huku wakidai ajira na maisha bora ni dhahili kuwa hujawaletea hayo maisha bora, ajira pamoja na kutekeleza kulitetea taifa lako kwa kushughulikia Mafisadi ili kuondoa umasikini iliokidhili kwa kila jamii.

Kwahiyo baada ya kuona maisha yao yanaendelea kudidimia huku wakiumia katika dimbi kubwa la umasikini wa kulala njaa na kuvaa nguo chakavu na zilizochanika kwa kukoswa pesa za kununua nguo mpya na chakula, wakamua kufanya jambo kama hilo ambalo halikutakiwa kutendeka.

Nakupa pole sana kwa misukosuko inayokupata katika uongozi wako Rais wangu, kwani uongozi wako umekuwa na misukosuko kila wakati tukiangalia misukosuko mingine tofauti na kurushiwa mawe na kuzomewa kule Mbeya.

Tunaona tangia watanzania tukukabidhi madaraka misukosuko imekuandama sana! Tulishuhudia kuvunjika kwa Baraza la Mawaziri kutokana na kujihudhuru kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowasa kwa kashifa ya Mkataba feki wa Richmond uliosababisha pesa ya walipa kodi kupotea bure.

Mara tu baada ya Richmond tukaona suala EPA nalo likaibuka ambalo lilisababisha pesa zetu kuchotwa pale benki kuu, Ndani ya utawala wako tu tumeshuhudia Zanzimbar iliyokuwa imara hapo zamani sasa inataka kujitenga.

Misukosuko inakuandama mara Madaktari kugoma wakidai nyongeza za mishahara, Wanafunzi wa vyuo vikuu kila wakati wanagoma wakidai hawatendewi haki mambo haya yote tumeyashuhudia, misukosuko inazidi kuendelea mara walimu kugoma wakidai malipo ya posho zao mpaka wanaamua kurusha mawe huku wakitoa machozi kama watoto wadogo kwa uchungu mkubwa.

Wazee wa walikuwa wa Wafanyakazi wa iliyokuwa Afirika Mashariki nao wanadai mafao yao ambayo bado wanaendelea kuzungushwa serikali yako, nao wanaamua kuzimalizia hisia zao kwa kumfungia Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi kwa hasira kali ya kuonyesha liwapo na liwe.
Jambo ambalo wazee hao wamelitoa juzijuzi katika viwanja vya Mnazi Mmoja Watanzania tunasononoka sana kwani katika viwanja hivyo wazee walisema kutokana na serika kushindwa kuwalipa mafao yao, sasa wamepanga kutoa pigo kali takatifu kwa serikali ambalo pigo hilo halitasahaulika daima! Japo kuwa hawa wazee walikataa kulitaja hilo pigo kwa waandishi wa habari wakidai kuwa serikali imekuwa ikipangua mipango yao wakiitaja, lakini hili pigo walisisitiza litakuwa la aina yake kwani serikali hata ifuatilie kwa aina gani haitagundua, bali itashutukia tu inapata pigo hilo takatifu.
Jamani watanzania tunashindwa kujua hili pigo takatifu ambalo serikali haitasahau litakuwa la namna gani? Lakini yote haya ni hasira ya wazee wale kunyimwa haki ya mafao yao wakati wakiona mafisadi wakiendelea kutanua na pesa za walipa kodi huku wakikumbatiwa na serikali kama vifaranga vya kuku.

Haya machache niliyoyatanja ni ishara tosha kabisa Rais wangu kuwa nchi yako inaelekea katika machafuko ambayo mwisho wake ni kuanguka kwa taifa la Tanzania.

Ukipenda nipigie: +255 764 992264
Niandikie: fitazi@hotmail.com

No comments: