Watanzania wanadhulumiwa haki yao |
TANZANIA ni nchi yenye kila aina ya rasilimali. Ina madini, misitu, mbunga za wanyama, maziwa mbalimbali kama vile Victoria, Nyasa, Tanganyika n.k. Vile vile ina Mlima Kilimanjaro ambao ni mlima mrefu kupita milima yote barani Afrika. Sifa nyingine ya nchi yangu Tanzania ni nchi ya amani kuzidi nchi nyingine ulimwengu kote. Ama kweli mimi ninajivunia kuwa Mtanzania. Ndiyo maana namwomba Mungu aibariki Tanzania. Tanzania ina sifa nyigi sana tangu zamani enzi za hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Nyerere aliitakia mema Tanzania, alitaka Tanzania yenye neema, Tanzania yenye kukua kiuchumi, kisaikolojia, kiutamaduni, kijamii na kisiasa. Lakini sasa hivi mbona mambo yamebadilika? Tanzania ya leo ipo tofauti sana na ile niliyoielezea hapo juu. Sasa hivi Tanzania inazizima, inawayawaya, inavunjika sana, inatumbukia shimoni, inanuka kila aina ya mabaya; kuna ufisadi, kuna EPA, kuna mpasuko wa kisiasa Zanzibar, kuna Richmond, kuna suala la Zanzibar ni nchi au si nchi, kuna suala la vijisenti vimefichwa Uingereza, kuna suala la Mkapa na mke wake kufanya biashara Ikulu ya Tanzania, na mengine mengi. Yote haya mbona Tanzania mnatuchanganya? Au mumeamua kufanya hivyo kwa sababu Baba wa Taifa hayupo? Au kwa sababu mlivunja Azimio la Arusha ambalo lilikuwa linabana na kudhibiti ufisadi? Mwalimu aliona mbali sana. Mlipovunja Azimio la Arusha ninawauliza mlitaka kila mtu ajichukulie chake? Kwa sababu ya nani haya yanatokea sasa? Tumlaumu nani kwa haya yote? Sasa mnatupeleka wapi, mbona sisi wananchi wa kawaida hatuwaelewi, mnaendelea kutuumiza! Sasa Watanzania wanalikumbuka Azimio la Arusha. Mwalimu aliona mbali sana kipindi cha utawala wake ndiyo maana alianzisha Azimio la Arusha. Aliona kuwa kunaweza kutokea watu wasiojali masilahi ya Watanzania wengine; walafi, mabepari, mabwenyenye, wenye fikra mbaya kwa wengine, wenye kutafuna taifa kwa kutumia dhamana ya uongozi na kusababisha Tanzania kuyumbayumba. Watanzania sasa wanamkumbuka Baba wa Taifa kwani wanaamini angekuwepo asingevumilia mambo kama haya ya ufisadi, ambayo alikuwa anayapiga vita sana kwa nguvu zake zote. Ninakumbuka Mwalimu baada ya kuona mambo kama haya ya ufisadi, unyonyaji n.k. yatatokea, bila ajizi aliitisha mkutano Arusha na kuanzisha Azimio la Arusha mwaka 1967. Lilipotangazwa, wananchi wanyonge wa nchi hii, walirukaruka na kushangilia. Wananchi hao walishangilia kwa sababu waliposikia misingi ya Azimio hilo, walifahamu fika kuwa ndio ukombozi wao. Walikuwa bado wana machungu kutokana na kunyonywa, kundamizwa, kunyanyaswa na kudhulumiwa ndani ya nchi yao wenyewe. Walikuwa bado wana kumbukumbu za ubeberu na ukoloni ambao ulikuwa umeota mizizi na pamoja na kuwa nchi ilikuwa huru, lakini watu wengi walikuwa bado hawajaanza kufaidi matunda ya uhuru, hasa katika nyanja ya uchumi, kwa sababu yalikuwa bado mikononi mwa watu wachache. Watanzania wanakumbuka Azimio lilisababisha kuzaliwa kwa siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Itikadi hii iliwawezesha Watanzania kushirikiana kwa kila jambo na hivyo kujenga udugu uliowafanya Watanzania wajione kuwa kama watu wa familia moja. Vilevile kujitegemea kulisababisha Watanzania kuishi kwa kujiona wao ni wao. Dhamira yao kubwa ilikuwa ni kujenga uwezo wao, ili waachane na utegemezi wa nchi nyingine. Walifahamu kuwa huo ndio uhuru wa kweli. Ili kuhakikisha kuwa linaondoa kabisa chembe chembe za unyonyaji, Azimio la Arusha liliweka kanuni zilizokuja kujulikana kama maadili ya uongozi kwa watumishi wa umma. Kanuni hizi zilitaja mambo ambayo mtumishi wa umma, hasa kiongozi, haruhusiwi kuyafanya. Hii ililenga kuhakikisha kuwa viongozi hawatumii nafasi walizonazo kujigeuza mabeberu, wakiritimba na wanyonyaji. Jamii iliwahakikishia viongozi kutunzwa kupitia mishahara yao. Pia dhana ya Ujamaa na Kujitegemea iliwahakikishia viongozi kuwa watakuwa sawa na wananchi wengine wanawaongoza. Azimio la Arusha lilizuia kujengeka kwa matabaka katika jamii ya walionacho na wasio nacho. Lakini hivi sasa nchi inayumbishwa na ufisadi, unyonyaji, ukandamizaji. Watu wameshaanza kumkumbuka Baba wa Taifa. Tunajiuliza tumekosea wapi? Inaleta hisia mbaya zaidi pale ambapo wanaoonekana kuwa vinara wa ufisadi na unyonyaji ni viongozi ambao tuliwakabidhi dhamana ya kutuongoza. Mwalimu ndani ya Azimio la Arusha na kanuni zake aliamini kuwa Watanzania wataishi kijamaa kwa kushirikiana kwa kila kitu. Alilenga kujenga umoja chini ya upendo wa kidugu. Katika mazingira kama hayo, kwenye dhamira ya dhati kabisa, isingekuwa rahisi kwa viongozi kuwageuka watu wao na kuanza kuwa wajasiriamali zaidi ya viongozi. Azimio la Arusha la Baba wa Taifa lilikataa ubaguzi wa mtu na mtu. Lilipinga unyonyaji wa mtu na mtu. Kitu hiki kilisababisha Watanzania kipindi hicho kuwa na amani katika maisha yao, huku wakiishi kwa kupinga aina zote za dhuluma. Lakini hivi sasa, amani hiyo ipo mashakani. Wananchi wa kawaida waliotopea katika umaskini wanapowaona viongozi wao wakiogelea katika ukwasi wa hali ya juu, huku wakihubiri umaskini, wanachanganyikiwa. Lakini viongozi wanapaswa kushikwa na hofu kwamba amani imeshaanza kutoweka. Unapoona watu wanamwadhibu kibaka aliyeiba kuku mtaani kiasi cha kufikia kumuua kwa kumchoma moto, ujue siku itafika ambapo watafanya hivyo kwa wezi wakubwa wakubwa na wala rushwa wakubwa wakubwa. Kwani lengo lao si ni kutoa adhabu kwa wahalifu? Viongozi wanatakiwa waanze kukaa chonjo hivi sasa. Vita dhidi ya ufisadi iliyoanza, haitakoma mpaka wananchi wa takaporidhika kuwa ushindi umepatikana kiasi cha kutosha. Salama ya viongozi ni kujiuliza nani alivunja hili Azimio la Arusha? Wanatakiwa kueleza kinagaubaga kwa nini Azimio lilivunjwa? Huyo aliyelivunja alikuwa anawatakia nini Watanzania? Aliyevunja azimio letu jema atuambie alikuwa ana makusudi gani kufanya hivyo? Hivi alikuwa anatutakia ufisadi, ubepari, ubeberu na mambo ya EPA? Au alitaka kuona Tanzania inawayawaya na kufikia hatua ya viongozi kuanza kufanya biashara Ikulu? Ndiyo. Haya yote yanatokea hivi sasa kwa sababu ya kuvunjwa kwa Azimio la Arusha kwani Azimio lilikuwa halitaki mambo haya yote. Hakika Mwalimu alikuwa anaipenda Tanzania, mbona hamkumuenzi Mwalimu? Mnataka kutuambia kumuenzi Mwalimu ni kufanya biashara lkulu na kumiliki migodi? Mbona Azimio la Arusha lilikuwa halitaki hivyo? Baada ya Mwalimu kung’atuka madarakani, tumeona yale ambayo alikuwa anayapiga vita yakianza kujitokeza taratibu na alipofariki yakashika kasi. Kasi ya mambo aliyoyachukia Mwalimu iliongezeka zaidi pale walipoamua kulivunja Azimio la Arusha. Wakati azimio hili lilitangazwa kwa mbwembwe zote mwaka 1967 wakati linazaliwa, lilipofutwa hata haikutangazwa! Walikutana kimya kimya wakasema Azimio linasababisha watumishi wa serikali wakose nyumba pindi wanapostaafu. Sasa tunagundua kuwa walikuwa na nia ya kuweka misingi ya kuiba mali ya umma wakati wakiwa kazini! Hao watu eti nao wanajiita wazalendo? Kutuvunjia misingi ya utawala bora ili muibe na kuwa mabepari, ndio uzalendo? Kuficha pesa katika benki za nje ndio uzalendo? Kujenga majumba makubwa kama mahekalu na kusomesha watoto wenu nchi za nje kwa pesa za walipa kodi ndio uzalendo? Tuelezeni Watanzania, huo ndio uzalendo wenye itikadi ya kufia nchi yako kwa kuitetea? Kwa mimi ninavyoamini uzalendo ni ile hali ya kuwa tayari kuifia nchi yako. Kwani katika Tanzania hii hamuoni wazalendo? Hamuwaoni kina Dk. Willibrod Slaa kuwa hao ndio wazalendo? Hamuoni kuwa wako mbele kutetea maslahi ya nchi yao? Hamuoni Baba wa Taifa kwa kuanzisha Azimio la Arusha kuwa alikuwa mzalendo? Hamuoni Edward Sokoine na kazi aliyoifanya kuwa ni mzalendo? Kwakweli mmetufikisha pabaya sana na tunasema hatutaki kuendelea kusikia mambo ya ubepari, unyonyaji, ufisadi, EPA, biashara za Ikulu, mpasuko wa kisiasa Zanzibar na matatizo chungu nzima. Makala hii imeandaliwa na mwananchi mwenye fikra za maendeleo. Anapatikana kwa simu: 0764 992264 |
JAMANI NIMERUDI TENA NILIKUWA MASOMONI
-
IMERUDI tena kwenye kibaraza chetu, karibuni sana nilikuwa nigeria nasoma
masters ya Journalism Curriculum Development and Designing nimemaliza
nimerudi T...
12 years ago