Oct 20, 2008

Nani ataikomboa upya Tanzania?

SIKUTAKA kuandika juu ya Ujamaa tena katika maisha yangu lakini baada ya kukaa na kufikiria kwa kina zaidi nikaona nitakuwa siwatendei haki Watanzania wenzangu ambao walifaidika na ujamaa katika kipindi cha Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hasa katika kuondoa unyonyaji, dhuluma na ubaguzi yakiwemo mafisadi, katika kipindi hicho ujamaa ulitumia itikadi za kijamaa za kuunganisha watu kwa pamoja katika kufanyakazi na kama mtu ataonekan hafanyi kazi ujamaa ulimuona mtu huyo kama kupe anayeishi kwa kunyonya jasho la wengine.

Pia nikaona kama nitaacha kuzungumuzia Ujamaa nitakuwa simutendei haki Baba yetu wa Taifa ambaye alikuwa Mwazilishi wa huo Ujamaa ndani ya Azimio la Arusha. Ili kumuenzi Mwalimu baba wa Taifa aliyeondoa unyonyaji kwa kutumia hilo Azimio la Arusha ambalo lilikuwa na hiyo siasa ya Ujamaa sikuona sababau ya kuacha kabisa kulizungumzia Azimio la Arusha na siasa yake ya ujamaa.

Kitu ambacho kilitaka kunisababisha nisizungumzie Ujamaa tena ni ile kauli ya Rais wangu Jakaya Mrisho Kikwete niliyoisoma katika gazeti moja la kila siku toleo la jumapili kuwa Mheshimiwa Rais wangu wakati akifanyiwa mahojiano na shirika la habari moja, Mwandishi wa shirika hilo alimuuliza swali kuwa anaizungumuziaje kuhusiana na nchi yake ni ya kijamaa? na anazungumuziaje ujamaa katika nchi yake? katika jibu lake Rais wangu alisema Siasa ya ijamaa katika nchi yake iwapo mtu yoyote atazungumuzia ujamaa ataonekana kama Mwendawazimu!!

Siku hiyo niliposoma hiyo habari nilishutuka sana na nikaa kufikiria kama kweli Mheshimiwa anaweza kusema kitu kama hicho kuwa mtu akizungumzia ujamaa ataonekana Mwendawazimu! Baada ya kufikiria nikahoji mimi mwenyewe ataonekanaje mwendawazimu wakati huyo viongozi wetu akiwemo Mh. Rais wangu wanasisitiza kumuenzi baba wa Taifa na kazi alizozifanya ikiwemo na ujamaa?


Pamoja na kuhoji hivyo lakini hakiri yangu ikachukua jukumu la kuamua kuacha kabisa kulizungumuzia Azimio la Arusha na siasa yake ya Ujamaa na Kujitegemea kwani nilifikiri nikiendelea kuzungumuzia mambo haya nitaonekana kama Mwendawazimu!! na ili nionekane mimi ni Mwerevu basi nisizungumzie kabisa hili Azimio la Arusha na Utawala wake ambao ulituletea matumaini na faida kubwa sana Watanzania enzi za Mwalimu Nyerere kwa kuwa ulitokomeza na kudhibiti wanyonyaji,wadhulumaji na wahujumu ambapo sasa ni maarufu kwa jina mafisadi.

Lakini tangia niamue kuacha kuuzumgumuzia huu ujamaa nimekuwa nikijiouna ninazidi kuwa mjinga na ujinga ndio unaongezeka kwani nimekuwa nikisahau kabisa kumuenzi baba yetu wa taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere pamoja na utawala wake ambao ulikuwa wa haki kwa kila Mtanzania.

Baada ya kukaa kimya huku nikifukria nikagundua kuwa kumbe kuzungumuzia ujamaa wa Mwalimu ni kujinyima haki yangu ya kumuenzi baba wa Taifa, hapo ndipo nikapata akiri kuwa kumbe nilipochukua jukumu la kuacha kuzungumuzia ujamaa ni sawa na kumunyima haki yake Mwalimu ya kumuenzi pia ni mojawapo ya kuwanyima haki watanzania wengine kujua mambo ambayo yalifanya na ujamaa kwa manufaa ya watanzania.

Baada ya kugundua hayo nikaamua hata kama waniite Mwendawazimu lazima kila sehemu ninapopita nitalizungumuza na kuhubiri misingi ya Azimio la Arusha na siasa zake za ujamaa na kujitegemea mbazo zilitusaidia watazania kufaidi raslimali zetu wenyewe kwani zilileta neema kubwa kwa watanzania wote.

Mwalimu bila hiana aliona kuwa mambo ya ya ufasadi yangetokea katika Taifa letu, aliona dhuluma ingetawala katika jamii, aliona unyonyaji ungekuwa ndio mfumo tawala katika taifa letu, aliona ubaguzi ungekuwa utamaduni ulitawala katika Taifa letu, aliona umma wa watanzania utakuja kushindwa kutumia raslimali zake kwa manufaa yao, hapo Mwalimu ndio aliona ili kujikinga na mambo haya aazishe Azimio la Arusha na misingi yake ya utawala bora.

Azimio hilo likawa na misingi madhubuti ya kutoruhusu kiongozi yoyote kujitwalia pesa ya umma kwa manufaa yake. Kwa leo nitaongelea zaidi faida za ujamaa ambao nilikuwa nimeamua nisiuhubiri kwa kuhofia kuitwa Mwendawazimu.

Tunajua kabisa ujamaa ulitokana na Azimio la Arusha ukiwa kama mojawapo ya siasa ambazo zilitakiwa kila mtanzania azifuate na kwa matendo na imani ili kujikomboa kiuchumi, kifikra, kiutumwa n.k.

Mwalimu aliweka kanuni za siasa ya ujamaa katika Azimio la Arusha ili kuweza kuwawezesha watanzania kuwa wajamaa, waishi kijamaa kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuleta maendeleo kwa pamoja pasipo kubaguana.

Ujamaa wa Mwalimu ulikataa ubaguzi wa mtu na mtu ndani ya jamii ukimanisha kuwa binadamu wote ni sawa na ndugu, kwahiyo hakuna binadamu ambaye yuko juu ya mwezake, hakuna binadamu ambayo anatakiwa kumiliki mali za Taifa na mwingine kutomiliki, ujamaa ulikuwa na na misingi ya kutokomeza unyonyaji kwa kuwafahamisha watanzania kuwa hakuna mtu ambaye anatakiwa kufanya kazi kwani ulibainisha kuwa misingi ya ujamaa ni kufanyakazi kwa pamoja na haukuruhusu kiongozi yoyote kujichotea pesa ya umma sehemu yoyote iwe benki kuu au sehemu yoyote kwani pesa hiyo ilihesabiuka kuwa ni pesa ya kila mtu yaani ya kijamaa kwa ajili ya maendeleo ya wajamaa.

Ujamaa haukuruhusu dhuluma katika sehemu yoyote kwani ulisisitiza kila mtu lazima afanye kazi kwa nguvu zake zote na nia yake yote, ili kuleta maendeleo ya Taifa, vilevile ndani ya siasa ya ujamaa dhuluma ilihesabika kama ni dhambi ambayo ilipaswa kukemewa na kila Mjamaa.

Ujamaa wa Mwalimu ulisisitiza watu kushikamana kwa pamoja bila kubaguana ndio maana ulikuwa ukiendana na maadamano mbalimbali ya mishikamano hasa watu wa kijijini bila shaka watakuwa wanayakumbuka maandamano hayo ambapo watu walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali zikiwemo za kujivunia ujamaa kuwezesha kuleta itikadi ya kukomesha unyonyaji, na kuondoa fisikoko waliozoea dhuluma bila kujishughulisha.

Ujamaa wa Mwalimu ulileta vijiji vya ujamaa ndani ya jamii watu waliondolewa katika makazi ya porini na kuhamishiwa katika sehemu moja na kuuda kijiji kimoja ulifanya hivyo ukiwa na lengo la kusisitiza mushikamano wa kuishi kijamaa na ulitaka huduma za kijamii zimufikie kila mtu kwa pamoja pasipo kumuhudumia wa sehemu moja na kuacha wa sehemu nyingine.

Katika kulitekeleza hili Mwalimu alihakikisha watu waliokuwa katika sehemu hiyo moja ya kijiji wanapata huduma za kijamii zikiwemo shule, zahanati, mpembejeo, ghara za kutunzia nafaka zao, sehemu ya karibu ya kuuzia mazao yao na huduma nyingine nyingi kwa pamoja.

Katika vijiji vya ujamaa ili kuinua zaidi kilimo Mwalimu aliamua kila kijiji cha ujamaa kipewe Makisai na majembe ya kukokotwa na Ng'ombe ambayo yalikuwa yakitumika kulimia katika mashamba yao ya ujamaa na wakipata mazao wanauza katika sehemu hizo husika.

Hakika katika ujamaa kulikuwa na faida nyingi sana ambazo zingine sitaweza hata kuzitaja kwani kitamaliza sehemu yote ya gazeti hili na kwa ajili ya faida hizi hata kama muniite Mwendawazimu kwa kuzungumuzia ujamaa wa Mwalimu niitine tu, na ninawahakikisheni ya kuwa sitaacha kumuenzi Mwalimu kwa kazi yake kubwa aliyoifanya kama hii ya kuanzisha siasa ya ujamaa wenye misingi ya kutoruhusu mtu kunyonywa jasho la nguvu zake.

Ninaimani kabisa ujamaa ulioleta fikra ya usawa ndani ya jamii mpaka leo hatuna ukabira hata kidogo ukikaa kwa wagogo wewe msukuma kama mimi unaoneka ni Mjamaa kama wao kwahiyo utapatiwa kila kitu, ikienda kwa kwa Wanyantuzu wewe ni Mkwele utapokelewa vizuri na wala hutabaguliwa hata kidogo kama huduma zote utapata yote haya ni kwa sababu ya fikra za Mwalimu za ujamaa za kumdhamini mtu hata kama katoka wapi kama unakitu mugawane sawa ndio fikra za kiujamaa ambazo zilikataa unafiki.

Na mpaka hapo mimi sione sababu za kuona kuwa ukizungumzia ujamaa utaonekana kama ni Mwedawazimu. Kama kweli ujamaa ni mwendawazimu kwani ulileta hasara gani kwa umma wa Watanzania? kwani kuwahamisha watu kutoka sehemu walizo kuwa wanaishi ili huduma za kijamii ziwafikie kwa pamoja ni jambo baya? Kuondoa ubaguzi kwa kuwaunganisha watu katika sehemu mbalimbali ili waishi kijamaa ni jambo baya? kusisitiza watu wafanye kazi kwa pamoja ni jambo ili kujikomboa kimaendeleo pasipokutegemea wawekezaji nalo ni jambo baya? Hakika sione hatia ya ujamaa! na sione kosa alilolifanya Mwalimu katika kuanzisha ujamaa!

Huu mfumo ambao umetawala wa ubepari faida zake kwa watanzania mbona hatuzijui? Sasa tunaona mali zetu watanzania zinamilikiwa na wachche huku watanzania walio wengi wanahangaika kwenye ndimbwi la umasikini kitendo ambacho mongozo wa ujamaa ulikuwa hautaki hata kidogo. Wachache wanaotumia nguvu ya pesa zao ndio wanaoendelea kujitwalia sehemu ya raslimali zetu huku watanzania masikini wakiendele kunyanyasika, kuteseka na kushinda njaa huku wakikumbuka mtetezi wa wanyonge Azimio la Arusha na siasa yake ya Ujamaa.

Wawekezaji nao wanachukua raslimali zetu kwa bei poa kwa mfano hayo madini yetu asilimia 97 yote wanachukuwa wao na kupeleka kwao ughaibuni huku sisi wazalendo wakitubakishia asilimia 3 tu ambayo ukilinganisha na udhamani wa madini yetu ni sawa na tunawapa bure.

Ujamaa ulipinga mtu kujimilikisha kitu au kumiliki kitu pekee yake kwa manufaa yake peke yake (binafsi) bali mtu alitakiwa kila kitu ni cha umma hakuna mwenye nacho lakini sasa umilikishaji binafisi umetufanya Watanzania wengi waliomasikini kukoswa haki yetu ya kumiliki, kama umma wa watanzania sasa uchumi wote wanamiliki wachache wenye pesa zao huku Watanzania masikini hawana kitu wanalia na umasikini wa kushinda njaa kila siku, kumbukeni hakuna kitu kibaya maishani kama kuishi kwenye nchi yako lakini uchumi wa nchi hiyo unakuwa siyo wako hii ni sawa na utumwa.

Kumbe sasa tumewagundua hila zao kwa Mwalimu za kulivunja Azimio la Arusha na misingi yake ya utawala bora! Hila hizi kumbe walikuwa hawautaki ujamaa kwa sababu ni Mwendawazimu. Sasa nianawauliza wakati Mwalimu yupo mbona hamukusema kuwa ujamaa ni uendawazimwi? Mbona Rais wangu Kikwete anamuzalilisha Mwalimu kwa kuita mfumo wake wa uongozi ni uendawazimu?
Hakika mimi ninapata hasira ninaposikia Mwalimu baba wa Taifa anaenziwa kwa matusi ya aina hiyo! Jamani hizi za kuita ujamaa uendawazimu si ni laana kubwa mno? Mbona munatuingiza kwenye laana kubwa namna hii? Acheni hizo kama mumechoka kutuongoza si bora mukajihudhulu kuliko kuanza kutoa matusi kwa Mwasisi wa Taifa letu! Tahadhali kuanzia sasa mukome kututukania Mwalimu wetu kama mulikuwa hamumupendi sisi tunampenda sana.
Na ninamalizia kwa kusema kuwa laiti kama Mwalimu Nyerere angekuja kuishi na Watanzania tena, angeamua kuikomboa Tanzania upya, kwani angesikitika kuona ujamaa wake aliouleta kwa ajili ya kuikomboa Tanzania na kutokomeza unyonyanyi ubaguzi na dhuluma unafananishwa na Mwendawazimu huku maisha aliyoyataka Watanania kuyafuata ili waishi kwa usawa na haki hayafutwi tena.

Angeikomboa upya Tanzania kwani asingevumilia kuona watanzania wanaendelea kuishi katika umasikini huku baadhi ya wachache wanaishi maisha ya kifahari kutokana na kuwawadhulumu haki ya rasilimali zao. Pia angeshangaa kuona ubepari ambao alikuwa anaupinga vita kali sana katika kanuni za Azimio la Arusha sasa ndio umekuwa Mfalme wa Tanzania.
Ni mimi mwendawazimu nipigie: 0764 992264
Niandikie: fitazi@hotmail.com
Kwa taarifa zaidi niblogu: http://www.fitalutonja.blogspot.com/

3 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Nimefurahi sana kusoma yaani kwa kweli uongozi wa sasa hata mimi sioni wanafanya nini na hawa watu wanaokuja katika nchi za watu wengine na kujifanya wao ndio wana pesa na wao ndio wamiliki nani kawaita. Unajua Kila siku nilikuwa ninajiuliza lakini hata hivyo sijapata jawabu.

Ni kwamba hakuna atakaye ikomboa Tanzania upya kama sio sisi wenyewe watanzania na tena watanzania wakereketwa.
Mnakumbuka maneno haya aliyoyasema baba wa Taifa. "Uongozi unaweza ukawa mzuri au mbaya, au usiojali, lakini kama watu wameamka na wanajitambua wenyewe, kutoshirikishwa kwa mawazo na tabia ya jamii hakutaendelea kwa muda mrefu."
Kwa hiyo kinachobidi kama hawa viongozi wanaona hawawezi kazi basi wawape waoweza au nakosea?

Fita Lutonja said...

Mwalimu akifufuka hakika ataishangaa Tanzania jinsi walivyoikondesha na kuibakiza mifupa tu. rasilimali zake wameuza kwa bei poa huku watanzania wakihangaika na dimbwi la umasikini wa kukoswa chakula na kuvaa nguo zilizo chanika. Hakika kwa haya Mwalimu asingenyamaza angeamua kupambana kwa nguvu zote kama alivyopambana kwenye kuleta uhuru ili kuikomboa tena upya tanzania kutoka katika haya aliyayaleta Kikwete

Fita Lutonja said...

Lakini ninaiona nyota ya matumaini inakuja kwa mbali na inaashiria ukombozi wa wanyonge Tanzania ndoto zangu zinaona neema inakuja kwa kasi kubwa sana siku za uonevu wao viongozi wetu zinaelekea kikomo.