Dec 27, 2008

Aleyevunja azimio la Arusha alimusaliti baba wa Taifa Mwalim Jk. Nyerere


Anasitahili kulaaniwa na Watanzania wote

Na Fita Lutonja

ILIKUWA mwaka 1992 kipindi cha rais Ally Hassan Mwinyi ambapo watu wachache bila hata kumshirikisha Muasisi wa Taifa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere walikutana Zanzibar wakiwa na lengo la kuvunja mwongozi alioweka Mwalimu wa Azimio la Arusha.

Mwaka huo ulikuwa ni mwaka wa mapinduzi makubwa yaliyofanya na watu hao yakuondoa mfumo wa utawala wa Azimio la Arusha ambao ulikuwa unakataza dhuluma kwa kila mtu na kusisitiza kufanya kazi kwa bidii ili kuweza kulikomboa taifa kutoka katika umasikini.


Hatukujua mfumo wenye asili ya kibepari waliutoa wapi? Na ulikuwana faida gani kwetu? Kwa sababu hawakutueleza faida za Mfumo huo kwa taifa letu na watanzania kwa ujumla.

Walidai kuwa wanaanzisha Azimio la Zanzimbar ambapo lengo lake hatukulijua lilikuwa ni nini? Au ilikuwa ni kuruhusu aina ya ufisadi ndani ya serikali hatukujua? au hilo Azimio la ZanzĂ­bar lilikuwa na maana gani mpaka likasababisha mfumo wa baba wa taifa wa Azimio la Arusha kuonekana halifai? Jama hizo za kulivunja Azimio la Arusha mpaka leo watanzania hatujui zilikuwa na lengo gani?


Kama kweli walivunja Azimio la Arusha kwa lengo zuri mbona hawakutueleza faida za Azimio hilo la Zanzibar, kama alivyotueleza mwalimu faida za Azimio la Arusha?

Mwalimu alielezea faida za Azimio la Arusha kwa njia mbalimbali ikiwemo kupitia vyombo vya habari, vipeperushi, pia aliandika vitabu mbalimbali zinazoelezea faida za Azimio la Arusha lakini nyinyi na Azimio lenu la Zanzimbar hatujaona hata kitabu kimoja kinachoelezea faida za Azimio la Zanzimbar?


Tunakumbua ilikuwa mwaka 1967 ambapo Mwalimu alibaini dhuluma, matumizi mabaya ya madaraka , unyonyaji na ubinafsi wa viongozi ndani ya serikali yake, jambo ambalo aliona litaipeleka nchi katika hali mbaya kiuchumi na kuleta matabaka ya kiunyonyaji.

Mwalimu kwa kuona nchi itakuja kuwa mfalme wa unyonyaji aliamua kuanzisha mfumo mpya wa utawala wa Azimio la Arusha ambalo lilifanikiwa kukomesha fisikoko, unyonyaji na waliozoea kudhulu jasho la wananchi na kunufaisha matumbo yao pia nao walikomeshwa.

Fisikoko na kupe wanyonya jasho la wezao walikuwa wamezoea kudhulumu kutoka katika jasho la wanyonge walikomeshwa kwelikweli.

Mwalimu kwa kuhakikisha dhuluma, unyonyaji, wizi, matumizi ya madaraka vibaya na ukwapuaji wa pesa ovyo unathibitiwa aliamua kuazisha utawala bora wa Azimio jambo ambalo lilileta haki na usawa wa kumiliki mali ya umma.


Watanzania tuliposikia Azimio la Arusha limetangazwa huku likiwa na misingi ya utawala bora wa kuthibiti unyonyaji na dhuluma tulishangilia kwa fifijo na nderemo tukijua sasa saa ya ukombozi kwa taifa imefika.

Furaha yetu kweli ilileta matunda mema kwa taifa na wananchi kwa sababu Azimio la Arusha lilihakikisha kila mtumishi wa serikali anatumia madaraka yake vizuri huku akifanya kazi kwa bidii na kufuata maadili ya uongozi ili kujenga uchumi wa nchi.

Viongozi wote ndani ya utawala wa Azimio la Arusha hawakuruhusiwa kuiba mali ya umma na kujiongezea mapato yao, bali walitakiwa kutumia mishahara yao katika kuendesha maisha.

Lakini nyinyi muliona mafanikio haya yaliyoletwa na Mwalimu kwa kupitia Azimio la Arusha hayafai, kama hayafai kwanini munahubili utawala bora wa Mwalimu? Huwa munamaanisha nini mnaposema tumuenzi baba wa Taifa huku mkipingana naye kwa kuvunja misingi ya utawala bora wa Azimio la Arusha?

Azimio lilihakikisha mali ya umma inalindwa kwa ajili ya watanzania na iwapo kama kiongozi atatumia mali ya umma vibaya alihesabiwa kuwa amehujumu uchumi wa nchi na hukumu yake ilikuwa kali mno ili kutoa fundisho kwa kiongozi wengine kutotenda makosa ya aina hiyo.

Mwalimu alikuwa mkali sana akiona kiongozi yeyote amehujumu mali ya umma jambo ambalo linajithihilisha pale serikali yake kwa kuzingatia misingi ya maadili kwa kiongozi wa umma iliamua kumhukumu waziri mmoja wa sheria kwenda jera miezi 12 na kuchapya viboko 24 hadharani.

Tukiangalia katika utekelezaji wa maendeleo tuliona Azimio la Arusha lilianzisha siasa ya ujamaa na kujitegemea ili kuhakikisha taifa linajikomboa kutoka katika umasikini.

Katika mfumo wa ujamaa tunaona ujamaa wa Mwalimu ulisisitiza kufanya kazi kwa bidii na nguvu zote bila kutegeana ili kuongeza uzalishaji na kupelekea kuinua pato la taifa.

Ujamaa ulikataa dhuluma na matumizi mabaya ya pato la wajamaa huku ukisisitiza kuwa kila pato linamilikiwa na wajamaa wote na hakuna ubaguzi wowote.

Lakini sasa hivi dhuluma, utumiaji wa madaraka vibaya, unyonyaji, ubaguzi, mikataba mibovu ya Richmond, uchotaji wa pesa za malipo ya nje (EPA) umezidi na kupelekea watanzania kuhujumiwa mali yao hadhalani jambo ambalo Mwalimu alikuwa akilipinga sana ndani ya utawala wake wa Azimio la Arusha.


Vilevile ndani ya Azimio la Arusha, Ujamaa ulikuwa na misingi ya kutoa huduma kwa jamii bure, ikiwemo huduma ya elimu, jambo ambalo lilipelekea kupata wasomi wengi tofauti na tulivyoacha na wakoloni ambao waliicha Tanzania ikiwa na wasomi wenye taaluma wachache.

Katika utekelezaji wa jambo hili unadhihilisha kuwa Mwalimu hakupenda kabisa dhuluma zitokee hata kwenye sekta ya elimu kwani kumlipisha mtu aliona itajenga matabaka kwa wasomi wenye pesa, na masikini wasikuwa na elimu.


Na katika siasa ya kujitegemea Mwalimu alisisitiza kufanya kazi kwa bidii bila kutegemea misaada kutoka katika mataifa mengine kwa sababu alijua kuwa sisi ni matajiri wa rasilimari nyingi ambazo tukizitumia tunaweza kujikomboa kiuchumi.

Hakika Azimio lilifanikiwa kukomesha hali ya dhuluma, unyonyaji, ukupe, fisikoko, wezi wa mali ya umma, ukiritimba, ubeberu wa kujimilikisha mali ovyo kisa umebeba madaraka, yote haya ndani ya utawala wa Mwalimu yalikomeshwa.

Lakini sasa watanzania tunadhulumiwa haki yetu kabisa tunashuhudia viongozi wanatumia madaraka vibaya na kujimilikisha mali ya umma huku wakidai kuwa ujasiliamali? Tuelezeni kama mlivunja Azimio la Arusha ili muwe wajasiriamali?

Hii kweli inaingia akilini kuwa ujasiliamali unaufanyia kwenye sehemu ya uongozi? Mbona Mwalimu wakati akiwa kiongozi hakufanya huo ujasriamali? Kwa sababu alikuwa anaheshimu utawala bora wa Azimio la Arusha ambao nyinyi muliona haufai.

Haki yetu mbona munachukua bira kutuhurumia sisi watanzania masikini? Munahubiri maisha bora kwa kila mtanzania, tutapataje maisha bora wakati misingi ya kulinda mali ya umma mumeivunja iliyokuwa inatekelezwa na Azimio la Arusha?

Tunajua kuwa Azimio la Arusha lilileta usawa na kuondoa matabaka ya matajili na masikini. Lakini sasa hivi tunashudia matabaka ya walionacho na wasionacho yameongezeka huku hao matajiri wakitudhulumu nguvu kazi zetu kwa kututumikisha na kutulipa ujira finyu jambo ambalo Mwalimu alikuwa analipinga sana.

Mumevunja Azimio la Arusha ambalo lilikuwa na misingi ya maadili kwa kiongozi wa umma kutojimilikisha na kutumia madaraka vibaya kujinufaisha mwenyewe lakini sasa hivi watanzania tunashuhudia kila kiongozi aliyoko madarakani anamiliki mali nyingi, kila kiongozi aliyestafu tunaona ndio wale wanaomiliki makampuni, taasisi pamoja na vitega uchumi vingi.

Hizo mali mumezipataje? Kama sio kuthulumu mali ya watanzania wezenu? Kama kweli mumepata kwa uhali mbona munalindana zikitolewa hoja za kuchunguzwa?

Wakina Wilbroad Slaa wakipendekeza muchunguzwe ili kubaini mulikozipata hizo mali, munaanza kujikingia kifua na kujilinda wenyewe ili msifichunguzwe. Hakika tunawaambia kuwa Mwalimu alipoanzisha Azimio la Arusha hakutaka kabisa mambo mnayoyafanya yafanyike ndani ya nchi hii ya Tanzania.

Hakika kama Mwalimu angerudi angeshaanga kuona Tanzania aliyoiacha imebadilika, wawekezaji, mabepari, mabeberu wakiritimba na viongozi ndiyo wamekuwa wamiliki wa rasilimali za watanzania, pia angeshaagaa kuona mikataba mibovu kama ya Richmond inayosababisha kupotea kwa fedha za walipa kodi, ikisainiwa na viongozi wa Tanzania ya sasa.

Angesikitika kuona pesa ya malipo ya nje (EPA) inachotwa na viongozi huku wakishirikiana na wafanyabiashara maarufu wakati watanzania wanalala njaa.

Angeshaangaa sana, kuona viongozi wanatumia ofisi za umma kama ngao ya kufanyabiashara huku wakijiita wajasiriamali, jambo ambalo Azimio lake lilikuwa linakataza.

Angewasikitikia watanzania kwa kuzongwa na umasikini unaosababishwa na kuvunjwa kwa Azimio la Arusha na utawala bora.

Pia angeamua kungana na watanzania wote wanaodhulumiwa jasho lao kuamua kuikomboa upya Tanzania ili kulisimika tena Azimio la Arusha litokomeze dhuluma, unyonyaji, ubeberu, ubepari, ufisadi, ukupe na wizi wa pesa za umma.

Watanzania tungeshangilia kuiona tena saa ya ukombozi imefika kwani tumeteseka sana, tumeonewa sana, tumedhulumiwa sana, na tunatamani sana kujikomboa.

Makala haya yameandikwa na Mwananchi mwenye fikra za kimaendeleo anapatikana kwa simu: 0764 992264.

MWISHO.