Sep 24, 2008

Ipo siku haki yetu itapatikana.


Aliyevunja Azimio la Arusha ana hatia kubwa

Makala

Fita Lutonja

NINAIKUMBUKA Februari 5, 1967 kama ni siku ya ukombozi wa wanyonge na changamoto ya kuongeza fikra za maendeleo miongoni mwa Watanzania, kwani siku hiyo kule Arusha, hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alitangaza kukomesha watu waliozoea kunyonya jasho la wanyonge bila huruma.

Hakika siku hiyo ilikuwa ya neema kwa Watanzania, kwani mfumo mpya wa utawala chini ya Azimio la Arusha, uliashiria nyota ya matumaini ya kujikomboa kwa wanyonge na waliokuwa wanadhulumiwa haki zao.

Baada ya Tanganyika kupata uhuru wake mwaka 1961 na kuwa Jamhuri mnamo mwaka 1962, na hatimaye kuungana na Zanzibar mnamo mwaka 1964 na kuunda Tanzania, hatukuwa na maendeleo makubwa.

Lakini Mwalimu kwa kuona baadhi ya viongozi kuwa bado wana fikra za kinyonyaji kama walizokuwa nazo wakoloni, akaamua kuanzisha Azimio la Arusha lililokuwa na misingi ya kulinda haki za wanyonge na kuondoa dhuluma ya tabaka la wanyonyaji.

Mwalimu aliona kipindi hicho umma wa Watanzania ukidhoofishwa kwa kudhulumiwa haki na tabaka la mabeberu na mabwanyenye ambao wengi wao walikuwa ni viongozi serikalini, kitendo hicho cha viongozi kuwanyonya wanyonge kilimkera sana.

Dhuluma haikuwa siri kipindi hicho, viongozi waliwadhulumu Watanzania waziwazi bila hata aibu, huku wakijiona wao ni bora zaidi ya wanyonge, wakiendelea kujikusanyia mirija mirefu ya kunyonya mali na haki za watu wengine. Waliendelea kuwakashifu walipa kodi kwa kuwanyonya jasho lao bila hata kuwahurumia.

Haikumchukua muda Nyerere kubaini kuwa ndani ya serikali yake changa, kuna wanyonyaji; mabepari na mabwanyenye ambao hawakuwahurumia wananchi wanyonge wa kawaida.

Alitambua kumbe ubepari na unyonyaji si rangi ya mtu tu. Ilionekana wazi kuwa hata watu weusi wanaweza kuwa wabaya kama walivyo Wazungu.

Baada ya kuona kuwa wanyonge wanadhulumiwa haki zao, tena hadharani, Nyerere aliamua kulinda haki yao ili isiendelee kudhulumiwa.

Aliunda Azimio la Arusha kama misingi ya kuhakikisha kuwa haki ya mnyonge inalindwa kama inavyolindwa haki ya mwenye nguvu. Aliliwekea Azimio kanuni za kuhakikisha hilo linatendeka.

Ni kweli kuwa Azimio lilisaidia kuleta usawa katika jamii. Kupitia Siasa ya Ujamaa, Azimio la Arusha lilifanikisha wanyonge nao kujiona kuwa wana fursa ya kufaidi matunda ya uhuru. Ujamaa na Azimio liliwataka viongozi kuwa wajamaa kweli, wakiwaona watu wanaowaongoza kama ndugu.

Hii ilisaidia kujenga utawala bora, unaoheshimu misingi ya utu badala ya unyonyaji. Hakukuwa na mtu dhalili na mtu bora. Unyonyaji ulionyeshwa kuwa ni mbaya.

Azimio la Arusha pamoja na misingi yake kwa watumishi wa umma, vilevile lilisisitiza ujamaa kuwa ni imani na njia pekee ya kuondokana na ubaguzi, ubinafsi na dhuluma, na kuwafaidisha wananchi wa aina zote nchini. Azimio, pamoja na Ujamaa viliamsha mori na ari ya kufanya kazi kiasi kwamba nchi ilifanikiwa kujijenga kwa kiasi kikubwa.

Watu walifanya kazi kwa kujitolea na kuanzisha vijiji vya ujamaa hadi viwanda. Tanzania ikageuka kuwa mzalishaji wa bidhaa zilizohitajika sana kwa ajili ya kusukuma gurudumu la maendeleo.

Azimio lilikuwa na siasa ya kujitegemea pia, ambayo iliboresha utumishi wa umma na uajibikaji wa viongozi na wananchi wa kawaida. Siasa hiyo ilimtaka kila mtu katika nafasi yake, kuhakikisha anazalisha kwa wingi, ili kuepuka kutegemea mtu mwingine.

Hii ilianzia kwa mtu mmoja mmoja mpaka kwa taifa. Taifa nalo lilitakiwa kujitegemea kwa mahitaji yake yote muhimu.

Watu walitakiwa kuwa na fikra kuwa wanaweza kuendesha maisha yao binafsi, au nchi bila hata kutegemea nchi nyingine. Tofauti na sasa, ambapo Azimio limeuawa, nchi imekuwa ni kama ombaomba. Jinsi ambavyo wanavyoongezeka ombaomba wa mitaani, na nchi nayo inazidi kuwa ombaomba na inakuwa kama inashindana na ombaomba wa mitaani.

Sasa hali imebadilika baada ya Azimio la Arusha kuuawa na kuzikwa. Hali imezidi kuwa mbaya na kwa hakika, aliyeliua Azimio la Arusha anastahili kubebeshwa lawama zote na hata ikibidi alaaniwe.

Mtu huyo anapaswa kubeba lawama zote kwa sababu amewasababishia mamilioni ya Watanzania maisha magumu.

Hivi sasa Watanzania wameshaanza kushuhudia unyonyaji na unyanyasaji ndani ya nchi yao wenyewe, licha ya kuwa walipata uhuru miaka zaidi ya 40 iliyopita.

Unyonyaji umerudi kwa kasi kwa njia ya uwekezaji.

Wawekezaji wamegeuka kuwa wanyonyaji ambao wanakamua mali za Watanzania bila huruma.

Watanzania, ambao nchi yao ina rasilimali zisizohesabika, leo wamekuwa wanyonge kama watu wanaoishi jangwani kusiko na kitu chochote.

Hadi hii leo sijaelewa nini ilikuwa misingi ya kuvunja Azimio la Arusha. Na misingi hiyo ilikuwa na masilahi gani kwa umma wa Watanzania?

Inashangaza kuwa wakati Azimio la Arusha lilipoundwa, wananchi walielimishwa maana na faida zake. Lakini walipoamua kulivunja, hawakutokea hadharani kueleza sababu za kufanya hivyo!

Mwalimu alifanya mikutano na kuchapisha vitabu na makala mbalimbali, yote akilenga kuwaelimisha wananchi wa kawaida kuhusiana na mfumo huu mpya wa maisha yao.

Lakini wenzetu hawakuona umuhimu wa kuwaeleza wananchi kwa nini waachane na mfumo wa maisha ambao wamekuwa wakiishi kwa miongo minne iliyopita.

Kimyakimya walikusanyika Zanzibar na kufanya maamuzi makubwa huku Watanzania wenyewe wakiachwa gizani. Kwa nini wananchi hatukuulizwa kabla ya kufikia uamuzi wa kuvunjwa kwa Azimio la Arusha? Au kwa nini mlipoamua kulivunja hamkurudi tena kwetu kutueleza ni kwa nini mmefikia uamuzi huo?

Au mlipoingia madarakani mliona hamupati nafasi ya kutuibia na kutunyonya haki yetu kwa sababu ya kanuni za Azimio la Arusha ziliwabana?

Kwani Azimio la Arusha lilikuwa na kasoro gani? Hivi kutetea haki za wanyonge nacho ni kitu kibaya? Mbona hamkutueleza hizo kasoro?

Azimio la Arusha, lililokataza viongozi kumiliki mali kupindukia limevunjwa na matokeo yake tumekuwa na viongozi mafisadi.

Au sijui ni mafisadi viongozi, maana ni vigumu kujua, kwa sababu wapo viongozi ambao walianza ufisadi kabla ya kupata uongozi na wakatumia mali zao kusaka uongozi, pia wapo viongzoi ambao walitumia nafasi zao kujilimbikizia mali na kuwa mafisadi.

Watu sasa wananyonywa na viongozi wao, dhambi ile ile ambayo Nyerere aliiona na kuiwekea kanuni za kuikataa.

Leo inakumbatiwa na wananchi wamekosa mtetezi kwa sababu viongozi ambao walipaswa kuwa watetezi wao, ndio wanaoongoza kundi linalowanyonya.

Azimio lenu la Zanzibar limeleta nini kwetu sisi Watanzania wa hali ya chini? Mbona limezidi kutuumiza na kutuletea maisha magumu na kutufanya tuwe wanyonge zaidi?

Sasa hivi masuala ya dhuluma, unyonyaji, umwinyi sanjari na ufisadi ndani ya serikali ni vitu vya kawaida.

Walidhani kuwa umaskini uliokuwepo ulikuwa unaletwa na Azimio la Arusha, wakaliua ili kutokomeza umasikini.

Lakini hali ya mambo imethibitisha kuwa hilo si kweli kwa sababu umaskini badala ya kutoweka, unaongezeka.

Na inavyoonekana ni vigumu sana kukuza uchumi wa nchi kwa mfumo walioukubali. Sana sana wanachofanya ni kujenga uchumi wa watu binafsi.

Tunatawaliwa kwa mfumo mpya wa ukoloni mamboleo. Tofauti yake na ukoloni tulioung’oa mwaka 1961 ni ndogo sana lakini madhara yake ni makubwa kuliko ya ule tulioukataa zamani.

Uhuru wetu sasa umegeuka kuwa wa bendera, jambo ambalo Azimio la Arusha lilikuwa linapiga vita kupitia kanuni zake.

Mwalimu katika mkutano wake wa kuelezea ubora wa Azimio la Arusha aliwaambia Watanzania ya kwamba jambo muhimu ni kujitegemea.

Aliwaambia Watanzania kuwa hawapaswi kumtegemea mtu mwingine yeyote. Tumeliua Azimio la Arusha na tumeingia katika mtego wa kuwategemea wafadhili na wahisani!

Azimio lenu la Zanzibar, ambalo kimsingi linatetea viongozi, limetuletea aibu ndani ya nchi yetu kwa viongozi wa umma kujimilikisha mali ya umma kwa kisingizio kuwa ni ujasiriamali.

Azimio lenu la Zanzibar tunalilaani kwa sababu limetuletea EPA, Richmond, unyonyaji, ubeberu, dhuluma, ufisadi, na matatizo chungu nzima ambayo yote haya tungekuwa na Azimio la Arusha yasingetokea kwani misingi yake ilikuwa hairuhusu.

Viongozi wanapswa kutambua kuwa wananchi wamechoka kweli na EPA, Richmond , unyonyaji, ubeberu, ubepari, ukupe, ukiritimba, umwinyi na wanachotaka ni Azimio la Arusha la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na misingi yake ya utawala bora, ili liunguze tena viongozi vikaragosi waliozoea dhuluma.

Idumu nguvu ya haki:
nipigie:0764 992264