Nov 24, 2008

Kunyongwa kwa Aleksander kaka yake Lenin ni hisia kubwa ya Lenin kutaka kuikomboa Urusi




Makala
KATIKA suala la kupigania haki za wanyonge kwa wakati mwengine linaweza kujitokeza kwa mtu kutamani kupigania haki za wanyonge kutokana na kuvutiwa na mtu furani ambaye anaonekana kuwa na harakati za kupigania haki ya wanyonge kwa nguvu zote.

Jambo hili lilitokea kwa mwanamapinduzi Mrusi mwenye fikra za kimaeneleo aliyejulikana kwa majina ya Vladimir IIyich Ulyanov (Lenin) ambaye kwa kiasi kikubwa aliathiriwa sana na kaka yake Aleksander ambaye alikuwa ni kijana mwenye nia imara mwenye kushirikilia maongozi mema ya kimaadili katika kuhakikisha wanyonge wanajikomboa.

Lenin alizaliwa Aprili 10 mwaka 1870, katika mji wa Simbirsk (sasa unaitwa Ulyanovsk) ulioko kwenye ng'ambo za mto Volga, na kukulia katika maeneo hayo ya wazi yaliyotanda sana ya mto huo mkuu wa Urusi, katika miji ya Simbirsk, Kazani na Samara.

Babu yake Lenini, N.V. Ulyanov alikuwa ni mkulima wa kitumwa wa Kirusi aliyekuwa akiishi katika Mkoa wa Nizhegorodsky, na katika mwaka 1791 alihamia katika Mkoa wa Astrakhan ambako aliandikiswa kama ni mtu wa tabaka la kati na alikufa katika hali ya umasikini hohehahe.

Baba yake Lenini, IIla Nikolayevich Ulyanov alikumbana na hali ya dhiki ya umasikini mapema sana maishani mwake, kaka yake ndiye aliyemsaidia mpaka akabahatika kupata elimu ya juu. Baada ya kuhitimu Chuo Kikuu cha Kazan baba yake Lenin alianza kufundisha katika shule za sekondari, na baadaye akawa Mkaguzi wa mashule na hatimaye kuwa Mkurugenzi wa shule za serikali katika mkoa wa Simbirsk. Alikuwa mtu mwenye fikra nzuri za kuleta maendeleo ya elimu kwa wananchi wa kawaida.

Mama yake Lenin, Maria Aleksandrovna, alitokana na ukoo wa daktari. Mama huyo alielimishwa nyumbani na akiwa mama hodari sana wa lugha nyingi za kigeni. alijua vyema fasihi na kupenda sana muziki. Alikuwa ni bibi Mwenye nia thabiti na tabia imara, mwenye akili, mtulivu na mwenye bashasha, alikuwa akijishughulisha sana katika kulea wanawe.

Katika ukoo wa Ulyanov kulikuwa na watoto sita ambao ni Anna, Aleksander, Vladimir, Olga, Dmitri na maria. Wazee wao walifanya wawezalo khakkisha watoto wao wanapata elimu ya fani mbalimbali, kuwalea wawe wapenda kazi, waaminifu, wenye adabu njama na wenye kuwafkiria watu wengine.

Kwahiyo Lenin alikulia katika ukoo huu ulioshikamana sana. Alikuwa ni mtoto mweye kuonekana wa furaha kila wakati huku akiwa mchangamfu, akipenda michezo ya hekaheka na ya makelele, kuogelea, kuteleza juu ya barafu na kwenda matembezini pamoja na marafiki wenzake.

Alijifunza kusoma alipokuwa na umri wa miaka mitano na alipotimiza miaka tisa aliingia darasala kwanza katika shule ya Simbirsk, wakati akiwa pale shuleni alisoma kwa hamu kuu akiwa na kipawa cha ajabu na kuyachukulia masomo yake bila mzaha wowote. Alikuwa kila mwaka akimaliza masomo anapata tuzo za hali juu kabisa.

Alikuwa tayari siku zote kuwasaidia wenzake pamoja na kuwafahamisha masomo magumu. katika madarasa ya mwisho ya sekondari aliwasaidia N. M. Okhotnikov, Mchuvash nk kujiandaa na mitihani yao ya kujipatia shahada ya kuhitimu shule.

Lenin mwanamapinduzi wa Urusi alikuwa akipenda sana kusoma na alivutiwa vizuri sana na vitabu vya A. Pushkin, M. Lermontonv, N. Gogol, I. Turgenev, N. Nekrasov, M. Saltykov-Shchedrin na L. Tolstoi. Sehamu kuu ya kisomo chake ilitawaliwa na vitabu vya wademokrati wa kimapinduzi, V Belinski, A. Herzen, N. Dobrolyubov na D .pisarev, pamoja na vitabu hivyo vilivyokuwa vimepigwa marufuku wakati huo. kitabu alichokuwa akikipenda zaidi ni cha N. Chernyshevski akiwa kama mwanchuoni mashuhuri na mpinzani mkali wa utawala wa mfalme na umwinyi.

Tabia na maoni ya Lenin ujanani mwake yalipatikana kutokana taathira ya malezi ya nyumbani, vitabu alivyosoma vya kimaendeleo pamoja na maisha yaliyokuwa yakimzunguka.

Wakati ule ubepari ulikuwa ikikua kwa kasi sana katika Urusi, makarakana na viwanda mbalimbali vilikuwa vikichipuka na kuajili wafanyakazi wengi ambao walikuwa wakinyonywa na kukandamizwa sana kitendo ambacho kilipelekea hali ya wafanyakazi hao kuwa mbaya sana kwani udhalimu wa serikali ya mfalme, mukandamizo wa makabaila, umasikini na unyonge wa wafanyakazi na wakulima yote haya yalimufanya lenin kuwa chukia wanyonyaji.

Lenin aliathiriwa sana na fikra za kaka yake, Aleksander ambaye alikuwa ni kijana mwenye nia imara ya kuhakikisha anaikomboa urusi kutoka katika tabaka wa wanyonyaji. "Mfano wa kaka yake kipenzi ulikuwa ni muhimu sana kwa Lenin," anasimulia Anna Ulyyanov dada yake Lenin, na kuongeza kuwa, tangu utotoni alijaribu kumwigiza kaka yake kwa kila jambo, aulizwapo atakuwa nani katika maisha yake, jibu lake lilikuwa: "Kama kaka yangu nimpendaye Aleksander"

Aleksander alikuwa ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha St. Petersburg na alikuwa na lengo kuu katika maisha yake la kuendesha mapambano ya kimapinduzi dhidi ya utawala wa kinyonyaji wa mfalme na kuupigania umma upate maisha mazuri.

Aleksander alikuwa akielekea katika mfumo wa Mwanaharakati wa kijamaa Karl Marx katika kuhakikisha umma unajikomboa kutoka kwa utawala wa kiunyonyaji wa mfalme, ilikuwa ni kutokana na kaka yake Aleksander ndivyo Lenin alipotambua kwa mara yake ya kwanza juu ya maandishi yafuatayo maongozo ya Marx.

Lenin alikubwa na mikasa mikali ya maisha wakati akiwa kijana mdogo kutokana na kufiwa na baba yake ghafla mnamo mwaka 1886, na mara ukoo huo haujafarijika kutokana na pigo hilo mara ghafla tena msiba mwingine wa kaka yake Aleksander ukaanguka.

Msiba wa kaka yake Aleksander ulitokana na mnamo Marchi 1887 Aleksander alikamatwa mjini St. Petersgurg akikabiliwa na shtaka la kuhusika na jaribio la kutaka kumuua mfalme Aleksander III, na katika Mei, mwaka huo huo Aleksander alinyongwa katika Ngome ya Schelisselburg. "Aleksander Ulyaniov amekufa shahidi" aliandika Anna, dada yake na kuongeza kuwa "roho yake iliyotolewa mhanga imekuwa kama mwenge wa kimapinduzi uliomwangazia njia ndugu yake, Lenin."

Kunyongwa kwa kaka yake kulikuwa ni pigo kubwa sana kwa Lenin na kuthibitishia moyoni nia yake ya kuyatoa mhanga maisha yake kwa mapambano ya kimapinduzi katika kuhakikisha anaikomboa Urusi kutoka katika unyonyaji. Pamoja na hayo Lenin aliona fahari kubwa kwa kaka yake kujitoa mhanga kwa kupigania wanyonge hapo ndipo alijawa na fikra za kuhakikisha anaikomboa urusi kama kaka yake alivyodhamilia kufanya.

Kutokana na Machungu ya kaka yake lenin akaamua kutafuta njia ya kufuata fikra za kaka yake katika kuhakikisha anaikomboa urusi, katika kujitayalisha kwa mapinduzi hayo kijana huyo alikuwa na hamu sana ya kujifunza elimu za kijamii. Katika Agosti 1887, baada ya kuhitimu elimu ya sekondari pamoja na kutuzwa nishani ya dhahabu, aliingia katika Chuo kikuu cha Kazan akichukua fani ya sheria hiyo no mojawapo ya njia za kuelekea kuikomboa urusi kwa kufuata njia za kaka yake kipenzi Aleksander.

Katika Chuo Kikuu Lenin Ulynov akaaza kuingiliana na wanachuo wa kimaendeleo, wenye fikra za kimapinduzi. Mwanzoni mwa Desemba 1887 alifukuzwa katika Chuo hicho kwa kushiriki katika mkutano wa wanafunzi akisisitiza mapinduzi ya wanyonge. Baadaye Lenin alihadithia mazungumzo aliyokuwa akizungumza na afisa wa polisi aliyekuwa akimuongoza kwenda gerezani: "Ina maana gani kufanya uasi, kijana?" Afisa huyo alimuuliza na kuongeza: "Kwani huoni kuna ukuta mbele yako?" Ndiyo" Lenin alijibu na kuendelea: "lakini ukuta wenyewe umeoza kabisa, ukiusukuma kidogo tu unaanguka." Haya yalikuwa majibu ya Lenin kwa kujiamini ikijua kuwa ipo siku ukombozi wa wanyonge utaangusha ukuta wa unyonyaji.


Lenin alifungwa kifungo ambapo katika kifungo chake alikuwa anahamishiwa katika sehemu mbalimbali ambapo ilifikia hatua akahamishiwa katika kijiji cha Kokushkino (sasa unaitwa Lenino), Mkoa wa Kazan huku akiendelea kuwa chini ya ulinzi, wakati akiwa huko alitumia muda mwingi sana kumkumbuka mwongozo wa fikra za kaka yake za kukomboa wanyonge kutoka katika kunyonywa.

Vilevile alitumia muda wake kusoma na kujielimisha zaidi, alihathia "Nadhani sijawahi kusoma na kujielisha katika maisha yangu, hata wakati nilipokuwa gerezani St. Petersberg na huko Siberia, sijawahi kusoma kama nilivyosoma wakati nikiwa katika kijiji cha Kokushkino" alisimulia Lenin na kuongeza: "Nikiwa katika kijiji hicho nilisoma na kumbuka Aleksander kwa kwa kupania mno yaani kutoka alfajiri hadi usiku wa manane."

Basi katika umri wa miaka kumi na saba kijana Lenin alikuwa ameshashika njia ya kaka yake Aleksander ya mapambano ya kimapinduzi dhidi ya utawala wa mfalme.

Makala haya yameandaliwa kutoka katika mitandao na vyanzo vya habari mbalimbali.

Nipigie: +255 764 992264

Nov 2, 2008

Migomo na Maandamano siku hizi Tz hapakaliki




CHAMA cha Wafanyakazi ni umoja wajumuiya ya wafanyakazi katika sekta yoyote iliyohalali na inayofanya kazi kulingana na taratibu za nchi, kwahiyo chama ni kama raia nchini aliye na haki ya kujipatia mali au haki yake, vilevile kutetea haki zake mbele ya baraza na kulindwa na sheria ya nchi.
Vile vile Chama kinauwezo wa kugoma, kuishtaki serikali, kampuni, taasisi au mwajili yoyote iwapo kitafuata misingi inayokubalika katika kudai haki yake, vilevile chama kama chama kinaweza kushitakiwa kama kitavunja kanuni na sheria zinazotakiwa.
Huko wingereza vyama hivyo vilijulikana kwa jina la "Trade Unions" , katika miaka ya 1835 ndipo vyama vidogovidogo vilipojiunga huko kuko wingereza na kufanya umoja wa vyama uliojulika kama "Grand National Consolodated Trade Unions" vikiwa na lengo moja la kudai haki za wafanyakazi.
Kwahiyo umoja huo mkubwa uliwatisha sana Wamiliki wa viwanda, serikali pamoja na matajiri wa huko ambapo kwa kuhofia nao waliamua kukishambulia vyama hivyo katika Baraza Kuu, ili kuvidhofisha na waendelee kuwanyonya wafanyakazi pasipo kuwa na ngao yoyote ya kujilinda.

Katika mashambulizi hayo ambayo yalipelekea kudhofisha vyama hivyo na kukoswa nguvu mnamo mwaka 1865 hatimaye yalitokea matata ya watu katika miji ya Sheffield na Manchester kati ya wafanyakazi na matajiri wao, ambapo ilipelekea serikali kuchukua jukumu la kuchunguza juu ya mtafaruku huo ambapo serikali baada ya kumaliza uchunguzi wake ilitangaza sheria mpya mwaka 1875 ambayo ilijulikana kama Hati au Mkataba wa vyama vya wafanyakazi huko wingereza.

Huo ndio ukawa ndio msingi wa sheria wa vyama vya watu wa kazi huko wingereza na katika nchi zilizo kuwa chini ya Dola ya Kiingereza. Katika sheria hiyo ugomaji uliruhusiwa na wanachama wa vyama hivyo waliruhusiwa kuwashawishi wenzao nao wagome kwa kuzingatia sheria na kanuni za ugomaji.
Na sasa katika karne hii vyama vya wafanyakazi ni vyama vilivyo halali kabisa katika nchi zote zilizo huru na katika kila nchi vyama vya wafanyakazi vya sekta mbalimbali zinaendelea kutetea haki za wafanyakazi ili kuondokana na kuonewa au kunyanyaswa na waajiri wao.
Katika nchi yetu Tanzania tuna vyama vya wafanyakazi vingi sana na vimesajiliwa kihalali vikiwa na lengo la kutetea maslahi ya wafanyakazi wa sekta husika, lakini pamoja na haya vyama hivyo vimekuwa vikitekeleza majukumu yao ya kulinda haki, amani utulivu wa wanachama hapa nchini kama inavyotakiwa.

Pamoja na utekelezaji wa haki hizo hivi karibuni Chama Cha Walimu Tanzania (CCW) kilitangaza kugoma nchi zima na mgomo huo ungefanyika oktoba 15 mwaka huu lakini kutokana na serikali kuhofia kuwa mgomo huo ungeleta hasara kubwa kwa taifa iliamua kwenda mahakamani kupinga mgomo huo ambapo mahaka kweli iliupinga mgomo huo.
Lakini siku ambayo walimu walitangaziwa kuwa mgomo wao umesitiswa pale katika viwanja vya Karimujee walipandwa na hasira kubwa mno ninaimani kila mtu alisikiana na kuona kwenye vyombo vya habari vulugu viliyokuwepo hapo Karimjee ambapo siku hiyo ilikuwa pia ni siku ya kumbukumbu ya kifo cha baba wa taifa kwa walimu siku hiyo ilikuwa ni siku ya majonzi na huzuni.
Baadhi ya walimu walilia kwa machungu makubwa utadhani ni watoto wadogo hakika mimi ambaye nilikuwa pale nikichukua habari nilipatwa na uchungu wa huruma kubwa sana kwa walimu wangu ambao walinifundisha mpaka kufikia hatua hii niliyonayo kuwaona wakilia hadhalani huku watoto wao wakiwaangalia.
Niliwahurumia walimu wangu kwa kukataliwa kufanya mgomo ambapo tunajua kabisa kuwa mgomo ni mojawapo wa njia ya kufikisha ujumbe ulidaiwa kwa siku nyingi bila mafanikio, lakimi baadhi ya walimu walitangaza kuwa wataendelea na mgomo baridi wa kutoingia madarasani na kama walimu wakuu watawalazimisha kuingia madarasani watawafundisha wanafunzi uongo.
Sasa serikali yetu mbona mpaka sasa hatujasikia kuwa walimu wetu wameshaanza kulipwa mafao yao? Si mulisema kuwa haichukui siku chache suala lao litakuwa limeshughulikiwa? Au munataka tena watangaze kugoma tena kwa kutokwenda shule tofauti na sasa ambapo wamefanya mgomo baridi wa kufundisha uongo.
Sisi watanzania bado tunajua kuwa hawa walimu bado wamegoma kwa kutumia mgomo baridi wa kufundisha uongo kwani serikali haijatueleza kama imefanya utafiti na kubaini kuwa walimu wetu sasa wanafundisha ukweli!
Tunajua watoto wetu bado wanafundishwa uongo kwa sababu walimu walisema watafundisha uongo mpaka hapo serikali itakapolipa mafao yao na serikali mpaka sasa haijalipa mafao yao.
Wazazi tunahofu kushindwa kufaulu kwa watoto wetu katika mitihani yao kwa sababu serikali haitaki kulipa mafao ya walimu ili watoto wetu wafundishi ukweli tunasikitika sana kwa kupuuzia suala zito kama hili au kwa sababu watoto wenu wako shule za kimataifa na wengine wako Marekani na Wingereza ndio maana hamjari watoto wetu sisi masikini. Munaona sawa tu waendelee kufundishwa uongo watoto wetu.
Kama Mwalimu mmoja aliyesema pale karimujee kuwa kama wakuu wao watawalazimisha kuingia madarasani watafundisha 1+1=0 na hesabu za mlinganyo watafundisha kama hesabu za majira ya nukita, hanuoni kuwa tunakoelekea ni kuua fikra za watoto na kuzalisha rasilimali watu ambao hawaendani na kazi wanazozifanya?

Si hayo tu hata walimu wanaweza kutafuta njia nyingine ya kudai haki yao kwani kule wingereza kipindi cha wafanyakazi kunyanyaswa kwa kunyimwa mafao yao, wafanyakazi hao walitafuta njia nyingine ya kudai haki yao ambapo wafanyakazi wa viwandani waliamua kuvunja vunja vifaa vya viwandani zikiwemo mashini na baadhi ya majengo na wengine waliamua kuweka chunvi katika mashine ili vioze ambapo mapambano haya yalijulikana kama “Luddism movement” 1811.Mapambano haya ya Luddism yalilitia hasa kubwa sanaTaifa la wingereza na kupelekea kushuka kiuchumi.
Sasa walimu wakiamua kutafuta haki yao kwa njia nyingine ambayo itakuwa ya hasara zaidi ya kugoma hapo mutasemaje? Wakiamua kufanya kama Luddism ya wingereza hapo mutasemaje?
Chondechonde tunawaomba walipeni walimu wetu mafao yao ili watoto wetu wasifundiswe uongo na kunusuru kutokea kwa mgomo mwengine wenye aina kama Luddism ya wingereza kwani hasara itakayopatika ni hasara ya watanzania wote kwani ndio walipa kodi ya maendeleo ya Taifa.
Ukipenda nipigie: +255 764 992264
Niandikie: fitazi@hotmail.com

Taifa linaangamia taratibu chukua hatua




SALAAM Rais wangu Jakaya Mrisho Kikwete, nakusalimia ewe mtukuka mwenye nyingi rehema, mwenye upendo na nchi yako na watanzania wote hakika unaupendo mkubwa na nchi yako ndiyo maana huachi kufanya ziara kuizungukia nchi yakoTanzania kila sehemu ili kujua hari ya watu wako mlezi wa Tanzania na juzijuzi ulikuwa Mbeya, haya yote ni kutokana na kuipenda nchi yako.

Nchi yako Tanzania nayo Mungu ameijalia sana kwani rasilimali za kila aina vyote ameipatia, Tanzania tuna madini ya kila aina yakiwemo dhahabu, almasi, ulanga, Tanzanite n.k.

Vilevile ina maziwa na mito ya maji ya kila aina likiwemo ziwa vicktoria ambalo linazalisha samaki aina ya sangara kwa wingi ambao wakazi wa kanda ya ziwa wanapata Mapanki kwa ajili ya kutumia kama mboga kwani minofu yote huwa inachukuliwa na wawekezaji tuliowapa wachukue ili watupatie pesa za kigeni kwa maendeleo ya taifa letu.

Pamoja na hayo vilevile nchi yako Mheshimiwa Rais ina Milima mingi ukiwemo Mlima Kilimanjaro ambao ni Mlima mrefu kuzidi Milima yote Afrika, Mlima huu huwa unatuingizia pesa nyingi za kigeni yote haya ni kutokana na Mungu kuijalia nchi yako Tanzania.

Rais wangu Tanzania yako ina rasilimali nyingi sana ambazo na sisi watanzania tunazitumia ili kujiletea maendeleo pamoja na kwamba wawekezaji ndio wamechukua sehemu kubwa ya rasilimali zetu lakini yote haya ni kuhakikisha taifa linapiga hatua kimaendeleo.

Rais wangu Jakaya nakupa pole sana kwa Masaibu yaliyokukuta kwani tangia ukumbwe na kimbunga cha kuzomewa na kurushiwa mawe huko Mbeya sijakusalimia na kukupa pole baba mlenzi, mtetezi wa wanyonge.

Pole sana Mtukufu mlezi wa rasilimali za taifa kwa manufaa ya kizazi kijacho hakika wewe ni Mkombozi wa Tanzania ndio maana tulikupa kura kwa asilimia kubwa huku tukishangilia kuwa wewe ni chaguo la Mungu.

Yawezekana na Mungu alikujua kuwa wewe ndiye utakuja kuwatetea Watanzania kuondokana na dhuluma, unyonyaji, na kukomesha ufisadi ndani ya nchi yako mpaka kipindi cha miaka yako mitano itakapoisha ili kuingia tena uchaguzi mwingine wa hapo mwaka 2010 ambapo pia ungemalizia yaliyobakia.

Nakupa pole Rais wangu kutokana na matukio yanayoiandama serikali yako kwa sasa ni ya kusikitisha mno kwa sababu yanaashiria kuwa nchi yako Rais wangu ipo kwenye dimbi la hatari kuelekaea katika hari isiyo ya kawada kwani fikra za watu na hisia zao wameanza kuzionyesha hadharani sijui ni kwanini wanapata msukumu huu mpaka wa kuamua kukurushia mawe Rais wangu na kufanya Migomo ya kila aina?

Rais wangu yakupasa kufikiria kwa kina jambo hili la kurushiwa mawe wakati ukiwa katika ziara yako Mkoani Mbeya kwanini watu wa huko walidhubutu kukurushia mawe? Hapa kuna kitu ambacho unatakiwa kukitambua mapema ili kukipatia ufumbuzi kwa haraka zaidi kwani kitendo cha kukuzomea na kukurushia mawe ni nguvu ya fikra ya watu hao ya kufikria kuwa hujawatendea kitu fulani ambacho ulitakiwa kukitekeleza.

Sasa baada ya kuona kuwa haki yao hawapati japo kuwa ile haki wanaijua kuwa ni yao kihalali sasa ili kufikisha ujumbe wa hisia za fikra zao wakaamua kukuzomea na kurusha mawe ili ujue kuwa hujawapatia kile walichokuwa wanakitaka.

Nikiwa kule Mbeya kama kawaida yangu ya kuchukua habari ili nihabarishe umma wa Watanzania wenzagu wenye nia ya kujua matukio yanayotokea katika dunia hii nilibahatika kushuhudia kuzomewa kwa Rais Kikwete katika maeneo ya Mwanjelwa, katika maeneo hayo wananchi walipouona msafara wa wake walitanda barabarani kuuzuia msafara huo wa Rais wakimtaka azunguze nao.

Lakini alipojitokeza wananchi walianza kupiga kelele wakizungumzia ufisadi huku wakisema kwa nini Rais hashughulikii mafisadi mbalimbali wakiwemo wa EPA wakati aliapa kuwa atailinda na kuitetea katiba ya nchi? Na baadhi ya watu wakihoji kuhusiana ahadi alizotoa za kuwapatia ajira na maisha bora.

Na katika kijiji cha Kanga Wilayani Chunya tukio la kurushiwa mawe msafara wake ni jambo ambalo halisitahili na la kushangaza, lakini Rais wangu alichukulia kama jambo dogo na kumtaka Mkuu wa Mbeya John Mwakipesile ambaye alionekana kufadhisha sana na jambo hilo kwa kumwambia kuwa, asifadhaike sana kwani yeye Rais watu wa Mbeya wanampenda sana.

Rais jambo hili ni jambo zito kwani wananchi hawa kuamua kukurushia mawe huku wakidai ajira na maisha bora ni dhahili kuwa hujawaletea hayo maisha bora, ajira pamoja na kutekeleza kulitetea taifa lako kwa kushughulikia Mafisadi ili kuondoa umasikini iliokidhili kwa kila jamii.

Kwahiyo baada ya kuona maisha yao yanaendelea kudidimia huku wakiumia katika dimbi kubwa la umasikini wa kulala njaa na kuvaa nguo chakavu na zilizochanika kwa kukoswa pesa za kununua nguo mpya na chakula, wakamua kufanya jambo kama hilo ambalo halikutakiwa kutendeka.

Nakupa pole sana kwa misukosuko inayokupata katika uongozi wako Rais wangu, kwani uongozi wako umekuwa na misukosuko kila wakati tukiangalia misukosuko mingine tofauti na kurushiwa mawe na kuzomewa kule Mbeya.

Tunaona tangia watanzania tukukabidhi madaraka misukosuko imekuandama sana! Tulishuhudia kuvunjika kwa Baraza la Mawaziri kutokana na kujihudhuru kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowasa kwa kashifa ya Mkataba feki wa Richmond uliosababisha pesa ya walipa kodi kupotea bure.

Mara tu baada ya Richmond tukaona suala EPA nalo likaibuka ambalo lilisababisha pesa zetu kuchotwa pale benki kuu, Ndani ya utawala wako tu tumeshuhudia Zanzimbar iliyokuwa imara hapo zamani sasa inataka kujitenga.

Misukosuko inakuandama mara Madaktari kugoma wakidai nyongeza za mishahara, Wanafunzi wa vyuo vikuu kila wakati wanagoma wakidai hawatendewi haki mambo haya yote tumeyashuhudia, misukosuko inazidi kuendelea mara walimu kugoma wakidai malipo ya posho zao mpaka wanaamua kurusha mawe huku wakitoa machozi kama watoto wadogo kwa uchungu mkubwa.

Wazee wa walikuwa wa Wafanyakazi wa iliyokuwa Afirika Mashariki nao wanadai mafao yao ambayo bado wanaendelea kuzungushwa serikali yako, nao wanaamua kuzimalizia hisia zao kwa kumfungia Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi kwa hasira kali ya kuonyesha liwapo na liwe.
Jambo ambalo wazee hao wamelitoa juzijuzi katika viwanja vya Mnazi Mmoja Watanzania tunasononoka sana kwani katika viwanja hivyo wazee walisema kutokana na serika kushindwa kuwalipa mafao yao, sasa wamepanga kutoa pigo kali takatifu kwa serikali ambalo pigo hilo halitasahaulika daima! Japo kuwa hawa wazee walikataa kulitaja hilo pigo kwa waandishi wa habari wakidai kuwa serikali imekuwa ikipangua mipango yao wakiitaja, lakini hili pigo walisisitiza litakuwa la aina yake kwani serikali hata ifuatilie kwa aina gani haitagundua, bali itashutukia tu inapata pigo hilo takatifu.
Jamani watanzania tunashindwa kujua hili pigo takatifu ambalo serikali haitasahau litakuwa la namna gani? Lakini yote haya ni hasira ya wazee wale kunyimwa haki ya mafao yao wakati wakiona mafisadi wakiendelea kutanua na pesa za walipa kodi huku wakikumbatiwa na serikali kama vifaranga vya kuku.

Haya machache niliyoyatanja ni ishara tosha kabisa Rais wangu kuwa nchi yako inaelekea katika machafuko ambayo mwisho wake ni kuanguka kwa taifa la Tanzania.

Ukipenda nipigie: +255 764 992264
Niandikie: fitazi@hotmail.com