Apr 9, 2010

UDOM Uchafu Kunuka



  • Wanafunzi wabaki yatima
  • Na Fita Lutonja
    CHUO kikuu cha Dodoma ni chuo kipya ambacho kimejaa misukosuko na mikasa ya kila aina. Kama wewe unaishi bali na huwa unakiona chuo hiki katika runinga basi huwezi jua mambo yaliyopo katika chuo hiki.

    Yawezekana pia huwa unakisikia kwenye vyombo vya habari mbalimbali vikisifiwa na viongozi wetu akiwemo rais wetu ambaye hachoki kukisifia kila anapoulizwa kuhusiana na serikali imeleta maendeleo gani hasa katika sekta ya elimu.

    Rais wangu mara nyingi amekuwa akionekana katika nyombo vya habari mbalimbali akiisifu serikali yake hasa katika kujenga chuo kikuu cha Dodoma.

    Hakika ni jambo zuri kukisifia kwani ni mojawapo ya kukitangaza ndani na nje ya nchi ili kiweze kujulikana zaidi ikiwa pamoja na serikali kupata sifa mbalimbali kwa kuamua kujenga chuo hicho.

    Lakini pamoja na kuangalia kwa umbo la nje basi wanatakiwa kuangalia na umbo la ndani ya chuo hicho, kwani chuo hicho kina kabiliwa na matatizo chungu nzima.

    Ukianzia tatizo la maji kwa wanafunzi hakika wanafunzi wanateseka sana nikiwemo na mimi mwandishi wa habari ambaye pia ni mojawapo wa wanafuzi wa chuo hiki.

    Katika chuo hiki maji huwa yanapatikana kwa shida wakati mwingine yanamaliza hata wiki mbili hadi tatu au zaidi bila maji na hapo chuo chote huwa kinanuka harufu mbaya kuanzia kwenye mabweni ya kulala mpaka majengo ya utawala.

    Wanafuzi wanaingia madarasani bila kuonga huku wengine wakikimbilia kijijini kwa wanakijiji kuomba maji angalu wapate ya kunawa usoni.

    Ni aibu kubwa sana kwa sisi tunaojivunia kuwa tumejenga chuo cha kimataifa wakati maji tu yametushinda kuyapeleka chuoni. Wanafunzi wanahangaika na maji wahadhili na wakufunzi wanahangaika na maji.

    Kwa upande wa wasomi wetu kuwatesa kiasi hicho cha kuwashindishi wiki mbili wakati mwingine wiki tatu bila maji tunajenga Taifa gani kwa vijana wetu? Au tunajenga Taifa la mateso? Kwa sababu tunajua kuwa vijana ndiyo Taifa la kesho.

    Mimi huwa nashindwa kujua hivi kweli uongozi wa chuo na wahusika wa maji tatizo hili hawalioni chuoni hapa? Kama maji Dodoma ni ya shida kunahaja gani ya kujenga chuo mahali ambapo hakuna maji kwa ajili ya wasomi wanaosoma hapo?

    Tusijenge chuo kwa kutafuta sifa bali tujenge chuo kwa kuangalia falsafa za mbele kwa kujiuliza. Je, hiki chuo kikiwa hakina maji kitazalisha wasomi wa aina gani? Je, iwapo kama wasomi wetu watasoma huku wakihangaika na kwenda kuomba maji kijijini watafaulu kwa kiwango kipi? Na je tunajenga chuo ili kije kilisaidieje Taifa kwa namna gani? Yatupasa tujilize maswali mengi na tukiyapatia ufumbuzi hakika hatuwezi kuwaacha wanafunzi waendelee kukoswa maji.

    Kitu kingine ambacho huwa kinanichanganya zaidi na kushindwa kujua kama kweli maji Dodoma hayapo ni pale viongozi wetu wanapokuja kutembelea chuoni.

    Siku hiyo ambayo kiongozi yeyote wa ngazi za juu kama anakuja chuoni maji huwa yanaanza kutoka kuanzia saa kumi usiku jambo ambalo huwa linaniacha kwenye dimbwi la fikra huku nikibaki na maswali ya kifalsafa; Kwanini yametoka?. Kwanini huwa wanakata maji kama hakuna kiongozi yeyeto ambaye anakuja chuoni? Kwanini sisi hawatudhamini wanatuona kama wanyama ambao hawaogi? Kwanini wanatutesa? Nk.

    Hivi karibuni wanafunzi tulikuwa tumechafuka kwa kukoswa maji lakini siku ambayo rais msitaafu ambaye pia ni mkuu wa chuo chetu Benjamin Mkapa alikuja chuoni tulipata nafuu kwani siku hiyo maji yalitoka siku nzima, lakini baada ya kuondoka tukaendelea na shida yetu ya kuishi bila maji huku tukivumilia harufu mbaya ya kila sehemu.

    Hapo sasa ndiyo tunajenga chuo cha kimataifa? Chuo bila maji wapi na wapi? Mzungu gani atakuja kusoma bila maji? Chuo bila kujali wanafunzi wapi na wapi? Chuo bila kujali wahadhili wake wapi na wapi? Tunajenga tu majengo lukuki lakini ndani hatuboreshi.

    Bila kuboresha ndani tutatoa wahitimu wanaokubalika kimataifa au tunataka kutoa wahitimu feki ambao wataenda kushindwa hata kufanya kazi ya taaluma walizozisomea na matokeo yake chuo chetu cha kimataifa kikaonekana na chenyewe feki?

    Siku ambayo alikuja Mkapa tulifurahi sana tukijua kwa kuwa yeye ni mkuu wa chuo basi tutamfikishia matatizo yetu ili ayapatie ufumbuzi ili nasi tupate nafuu ya kutulia chuoni kusoma badala ya kila siku kushinda tunahangaika vijijini kutafuta maji.


    Lakini siku hiyo cha kushangaza na kusikitisha ikiwa pamoja na kusitaabisha mkuu wetu wa chuo Mkapa hakuweza hata kuongea nasi, jambo ambalo lilituuma sana na kutuumiza roho zetu kwa kushindwa kufikisha shida zinazotukabili.

    Tukiangalia naye makamu mkuu wa chuo Prof. Idris Kikula naye hatupi nafasi hata ya kuonana naye ili angalau tuweze kumueleza shida zetu. Sasa sisi tutatatuliwa na nani matatizo yetu? Na tutaendelea na matatizo mpaka lini? Mbona munatudhulumu haki yetu? Mbona uhuru wetu munatunyima? Mbona munatuumiza kisaikolojia? Sasa iko wapi haki yetu? Kikula na Mkapa rais wagu mstafu na mkuu wangu wa chuo iko wapi haki na demokrasia yetu?

    Tangia nifike chuoni hapa yapata miaka miwili sasa lakini makamu mkuu wa chuo changu hajawahi hata siku moja kuongea na wanafuzi ili wamueleze matatizo mbalimbali yanayowaandama jambo ambalo huwa linatusikitisha.

    Yawezekana makamu wa chuo chetu katususia? Na kama katususia tumemukosea nini makamu wetu wa chuo Kikula? Tunamuomba sasa atuokoe na jahazi linalotukabili la mateso makubwa yanayotishia kutuharibia masomo yetu kwa kushinda nje ya chuo tukilandalanda kutafuta maji.

    Namkumbuka makamu mkuu wa chuo kikuu cha Dar es Salaam Prof. Rwekeza Mukandara huwa anaongea na wanafuzi mara kwa mara ili kuweza kujua matatizo yao mbona Pro.Kikula wa chuo chetu haongei na sisi wanafunzi wake?

    Wakati sijaja hapa chuoni kusoma nilikuwa naitumia taaluma yangu kwa kuadika katika gazeti la Mwananchi nimeandika habari nyingi za Mkandara akiongea na wanafunzi mpaka nimeondoka kuja kusoma huku Dodoma Mkandara alikuwa na huo utaratibu wa kuongea na wanafunzi. Mbona Kikula ambaye anaonekana baba mpole mwenye hekima na busara hafanyi hivyo?

    Sasa sisi wanafunzi wa Udom tumekuwa yatima hatuna wa kutusaidia ili kuondokana na matatizo haya. Tumetelekezwa bila msaada wowote na sasa hatuoni uhuru wetu shahada zetu ziko hatarini. Ninaishia hapa ili niwahi kwenda kijijini kutafuata maji iusije ikala kwangu.

    Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa simu: 0764 992264,niandikie:fitazi@hotmail.com Nitembelee: http://www.fitalutonja.blogspot.com/
    MWISHO